Maswali yaulizwayo kuhusu Opus Dei, Sehemu ya kwanza (Toleo jipya)

Kwa ajili ya ndugu na dada zetu katika Afrika Mashariki ambao wamekuwa wakitamani sana maandishi na rasilimali katika lugha ya Kiswahili, tunawatolea sehemu ya kwanza ya makala fupi inayoeleza Opus Dei. Rasimu hii ya kipeperushi imetafsiriwa kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na Dk. Walter M.Mbunda.

Photo by 愚木混株 cdd20 on Unsplash

Opus Dei ni nini?

Opus Dei ni utume wa hali ya juu wa mtu binafsi katika Kanisa Katoliki.

Dhamira yake ni kueneza ujumbe kuwa Wakristo wote wanaitwa na Mungu ili kumfanya Yesu Kristo ajulikane na kutafuta utakatifu ndani ya na kwa kupitia kazi zao za kila siku, maisha ya familia na uhusiano katika jamii.

Ili kuwasaidia watu kuuishi utume huu, Opus Dei inatoa malezi maalum ya kiroho kupitia mafunzo madarasani, mazungumzo, ushauri wa kiroho, mafungo, n.k. Utaratibu huu wa kiuchungaji unaimarisha uweza na fadhila za kuuishi Ukristo na kusisitiza kushiriki katika kazi ya Mungu ya uumbaji na ukombozi kwa kufuata mfano wa kazi wa Kristo uliofichika. Kazi anayofanya mtu inabidi ifanyike vyema kwa upendo wa Mungu na ionekane kuwa ni huduma kwa wote wanaoguswa nayo. Opus Dei’ ni jina lenye maneno ya lugha ya Kilatini yakimaanisha “Kazi ya Mungu”.


Unajiungaje na Opus Dei?

Ili kujiunga na Opus Dei kunahitaji mwito usio wa kawaida. Ni mwito kwa mtu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili aweke rehani maisha yake yote kwa Mungu, akihubiri ujumbe wa utakatifu kwa mataifa yote katika maisha ya kawaida na maisha ya kijamii.

Watu hujiunga uanachama kwa kuweka makubaliano ya mkataba badala ya ahadi za nadhiri, na hubakia kama walei wa kawaida katika majimbo yao. Wito huu wa kujiunga na Opus Dei kwa kawaida humaiziwa baada ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za Opus Dei (k.m mafungo, mafunzo, maelekezo ya kiroho) mara nyingi kwa kipindi kirefu, ambazo humwezesha mtu kujipatia elimu bobezi kuhusu Opus Dei. Ni muhimu vilevile kujipatia msimamo unaodumu kuhusu maudhui ya Kikristo ambayo wanaojiunga wanaahidi kuyafuata: kupokea Sakramenti mara kwa mara; kusali, utume na kwa ujumla unyenyekevu na juhudi endelevu ili kujipatia fadhila na kutafuta utakatifu kulingana na msimamo wa Opus Dei.

Bila kuwa na kipingamizi chochote kile, Watu wazima wakatoliki, wakiwa wanaume au wanawake, walioolewa au wasioolewa, wanaotoka katika jamii yoyote ile, taifa lolote au hali yoyote ya kiuchumi wanaweza kujiunga na Opus Dei.


Kwa nini Kanisa iliichagua Opus Dei iwe ya Utume wa Juu sana wa binafsi?

Tume za Juu za Binafsi ni mamlaka au miongozo ya Kanisa iliyotokana na Mtaguso wa Pili (Second Vatican Council) na Kanuni za Sheria ya Canon (Code of Canon Law) zinazotengenezwa ili kukidhi mahitaji maalumu ya kiuchungaji kwa urahisi. Opus Dei inaunganisha katika taasisi moja mapadre na walei, wanawake na wanaume, wenye wito mmoja wa kueneza ukamilifu wa utakatifu duniani na utakatifuzaji wa kazi. Kwa vile ni utume binafsi, hata hivyo, “inatoa fursa yenye mtazamo wa kikanisa kwa Opus Dei pamoja na misingi ya muundo wa sosholojia” (taz. The Holy See’s 1982 “Declaration on Opus Dei”).


Je, kuna uanachama aina mbalimbali wa Opus Dei?

Waamini wote katika Prelature wanashiriki mwito sawa wa kueneza ukamilifu wa utakatifu duniani kote. Wanachama wengi wameoa/wameolewa na wanajitahidi kumfuata Yesu Kristo kwa kutakasa kazi zao ndani na nje ya majumba yao, kupalilia roho ya upendo, kuwapokea kwa ukarimu watoto waliopewa na Mungu, kuwaelimisha watoto vyema na kusambaza imani kwao pamoja na ukarimu na kwa mifano. Kwa minajili ya uinjilishaji, baadhi ya Walei wanaume na wanawake wanazingatia useja kama zawadi kutoka kwa Mungu. Hii inawawezesha kujitoa zaidi kwenye kazi za kujiimarisha, bila ya kubadili taswira ya utume wa ulei wao, utaalamu walio nao, au nafasi zao katika Kanisa au kwenye jamii.