The conversion of the children of God (Kiswahili)

A homily of St. Josemaria for lent in Kiswahili from Christ is passing by: Uongofu wa watoto wa Mungu.

Audio

57 Tuko mwanzoni mwa Kwaresima: wakati wa toba, utakaso na uongofu. Sio utaratibu mwepesi, lakini hata hivyo Ukristu sio njia rahisi ya maisha. Haitoshi kuwa katika Kanisa, kuruhusu miaka ipite. Katika maisha yetu, katika maisha ya Wakristo, uongofu wetu wa kwanza - wakati ule wa pekee ambao kila mmoja wetu anakumbuka, ulipoelewa wazi wazi kila alichokuwa akikitaka Mungu kwetu – ni dhahiri kwamba ni muhimu sana. Lakini maongofu yanayofuata ni muhimu zaidi na yanaenda yakiitisha juhudi zaidi. Ili kurahisisha kazi ya neema katika maongofu haya, tunapaswa kuweka roho yetu katika hali ya ujana; inatubidi kumwomba Mungu, kujua namna ya kumsikiliza na, baada ya kujua kosa lililofanywa, tujue jinsi ya kuomba toba.

"Mkiniomba, nitawasikiza,"[2] tulisoma katika liturjia ya Jumapili hii. Si jambo la kushangaza jinsi Mungu anavyotujali na alivyo tayari kutusikiliza — akingoja mwanadamu aseme? Anatusikia kila wakati, lakini hasa sasa. Moyo wetu utayari, na tumenuia, kujitakasa. Anatusikia na hatapuuza ombi la “moyo ulio mnyenyekevu na wenye majuto."[3]

Bwana anatusikiliza. Anataka kuingilia kati na kuingia katika maisha yetu ili kutukomboa kutoka kwa maovu na kutujaza mema. "Nitamwokoa na kumheshimu,"[4] anasema kuhusu mwanadamu. Kwa hiyo, tunapaswa kuwa na tumaini la utukufu. Hapa kwa mara ingine tuna chanzo cha mwendo unaotunga maisha yetu ya kiroho. Matumaini ya utukufu yanatuzidishia imani yetu na kukuza upendo wetu; fadhila tatu za kitheolojia, fadhila za kimungu ambazo zinatufanya kama Baba yetu Mungu, zimeanza kazi.

Njia ipi bora ya kuanza Kwaresima? Tuifanye mpya imani yetu, tumaini na upendo. Roho ya toba na hamu ya utakaso hutoka kwa fadhila hizi. Kwaresima sio tu fursa ya kuongeza mazoea yetu ya nje ya kujinyima. Ikiwa tulifikiri ni hiyo tu, tungekosa maana ya kuu iliyo nayo katika maisha ya Kikristu, kwa sababu mazoea haya ya nje ni - kama nilivyosema - matokeo ya imani, tumaini na hisani.

Usalama hatari wa Wakristu

58 "Yeye aishiye katika msaada wa Aliye Juu kabisa, atakaa chini ya ulinzi wa Mungu wa mbinguni."[5] Huu ndio usalama hatari wa Mkristu. Ni lazima tuamini kwamba Mungu anatusikia, kwamba anatujali. Tukifanya hivyo, tutakuwa na amani tele. Lakini kuishi na Mungu kweli ni kazi ya hatari, kwa vile hataki mgawanyo wa vitu: anataka kila kitu. Na tukimsogea, itamaanisha kuwa tayari kwa uongofu mpya, kuwa na mwelekeo mpya, kusikiliza kwa makini zaidi ushauri wake — shauku takatifu anazoziwasha katika kila nafsi - na kutekeleza.

Tangu uamuzi wetu wa kwanza wa kufuata mafundisho ya Kristo kwa dhati, bila shaka tumepiga hatua nzuri katika njia ya uaminifu kwa neno lake. Hata hivyo, si kweli kwamba bado kuna mengi ya kufanya? Je, si kweli, hasa, kwamba bado kuna wingi wa kiburi ndani mwetu? Tunahitaji, bila shaka, kugeuka tena, kuwa waaminifu zaidi na wanyenyekevu, ili tusiwe na ubinafsi na kumruhusu Kristo akue ndani yetu, kwa maana, "Sharti aendelee kukua, nami niendelee kupunguka."[6]

Hatuwezi kutuwama. Ni lazima tuendelee mbele kuelekea lengo analosema Mtakatifu Paulo: "Si mimi ninayeishi, bali ni Kristo anayeishi ndani yangu."[7] Hii ni shauku kuu na tukufu kabisa, kujitambulisha na Kristo, utakatifu huu. Lakini hakuna njia nyingine endapo tunataka kujipatanisha na maisha ya kimungu ambayo Mungu amepanda rohoni mwetu katika ubatizo. Ili tuweze kusonga mbele, hatuna budi kujiendeleza katika utakatifu. Kukwepa utakatifu kuna maana kwamba tunayanyima maisha yetu ya Kikristu kukua ipasavyo. Moto wa upendo wa Mungu hauna budi kuchochewa. Ni lazima uongezeke kila siku kwa nguvu katika nafsi yetu; na moto unachochewa kwa kuongeze vitu zaidi vinavyoshika moto. Tusipouchochea, unaweza kuzima.

Kumbuka aliyosema Mtakatifu Agostino: "Ukisema 'tosha', umepotea. Songa mbele, endelea kusonga mbele. Usibaki pamoja, usirudi, usichepuke."[8] Kwaresima inapaswa kutudokezea maswali haya ya msingi: Je, ninapiga hatua katika uaminifu wangu kwa Kristu, katika haja yangu ya utakatifu, katika utume (kwa ukarimu) katika maisha yangu ya kila siku, katika kazi yangu ya kawaida miongoni mwa wenzangu?

Kila mmoja wetu anapaswa kujibu maswali haya, kwa kimya, na ataona kwamba anahitaji kujigueza tena ikiwa Kristu ataishi ndani mwake, endapo atataka tabia yake iwe na sura ya Kristu. "Kama mtu yeyote ana nia tuandamane, na aachane na ubinafsi, na achukue msalaba wake kila siku na kunifuata."[9] Kristu anatuambia haya kwa mara ingine, akitunong'onezea masikioni mwetu: msalaba kila siku. Alivyonena Mtakatifu Yerome: "Sio tu wakati wa mateso au wakati tunapobahatika kuwa mashahidi, bali katika kila hali, katika kila tutendacho na kuwaza, katika kila tusemalo, tukatae kile tulichokuwa na tukiri tulivyo sasa, watu tuliozaliwa upya katika Kristu."[10]

Ni mwangwi wa maneno ya Mtakatifu Paulo: "Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana. Ishini kama wazaliwa wa mwanga. Ambapo mwanga una athari zake, watu wanatembea na maadili, utakatifu na ukweli, wakitafuta vitu vile vinavyompendeza Mungu."<a id="m_-4567737825678559961__ftnref11"></a>[11]

Uongofu ni kazi ya muda mfupi; kujitakatifuza ni kazi ya kudumu maisha. Mbegu ya kimungu ya hisani, ambayo Mungu amepandikiza katika nafsi zetu, inataka kuchipua, kujionyesha katika matendo, kutoa matunda ambayo daima yanaambatana na matakwa ya Mungu. Kwa hiyo, hatuna budi kuanza tena, kugundua tena - katika hali mpya - nuru na kichocheo cha uongofu wetu wa kwanza. Na hii ndiyo sababu inabidi tujitayarishe kwa upekuzi wa kina wa dhamiri, tukimwomba Bwana wetu msaada wake, ili tumjue yeye na sisi wenyewe vizuri zaidi. Tukitaka kuongoka tena, hakuna njia nyingine.

Huu ndio wakati wa msamaha

59 "Tunakusihi usiipe neema ya Mungu mapokezi baridi."[12] Naam, neema ya Mungu inaweza kutujaa Kwaresima hii, mradi tu tusifunge milango ya moyo wetu. Hatuna budi tuwe na nia njema, tutake kwa dhati kubadilika; hatuwezi kucheza na neema ya Mungu.

Sipendi kuzungumza juu ya hofu, kwa maana Mkristu anafanyizwa na upendo wa Mungu, ambao umedhihirishwa kwetu katika Kristu na anatufundisha kuwapenda watu wote na viumbe vyote. Hata hivyo, tunapaswa kuzungumza juu ya kuwajibika, kuyapa mambo uzito yanayostahili. “Wala msijidanganye; hamwezi kumhadaa Mungu,”[13] Mtume Paulo anatuonya.

Tunapaswa kuamua. Haifai kuwa na mishumaa miwili inayowashwa - mmoja kwa Mtakatifu Mikaeli na mwingine kwa shetani. Sharti tuuzime mshumaa wa shetani: inatupasa kuyatumia maisha yetu kikamilifu katika kumtumikia Bwana. Ikiwa hamu yetu ya utakatifu ni ya kweli, kama tuwaelekevu vya kutosha kujiweka mikononi mwa Mungu, kila kitu kitaenda sawa. Kwa maana yeye daima yu tayari kutupa neema yake, hasa wakati kama huu - neema kwa uongofu mpya, hatua nyingine mbele katika maisha yetu kama Wakristu.

Hatuwezi kuichukulia Kwaresima hii kama majira mengine ya liturjia yaliyorudi tena. Ni wakati wa kipekee: msaada wa Mungu ambao tunapaswa kuupokea. Yesu anapita na anatumaini kwamba tutachukua hatua kubwa mbele - leo, sasa.

"Huu ni wakati wa msamaha; siku ya wokovu imeisha fika."[14] Kwa mara nyingine tena tunasikia sauti ya mchungaji mwema akituita kwa upole: "Nimekuita kwa jina lako."[15] Anamwita kila mmoja wetu kwa jina lake, jina tulilozoea linalotumiwa tu na wale wanaotupenda. Maneno hayawezi kuelezea upole wa Yesu kwetu.

Hebu fikiria maajabu ya upendo wa Mungu. Bwana wetu anakuja kutulaki, anatusubiri, yu kando ya njia ambapo hatuwezi kukosa kumwona, na anamwita kila mmoja wetu binafsi, akizungumza nasi juu ya mambo yetu wenyewe - ambayo pia ni yake. Anatuelekeza tujute, anafungua dhamiri yetu ili tuwe wakarimu; anatutia moyo tutamani kuwa waaminifu, ili tuweze kustahili kuitwa wafuasi wake. Tunaposikia maneno haya ya undani ya neema, ambayo yanatolewa kwa madhumuni yenye upendo, tunatambua mara moja kwamba Bwana wetu hajatusahau wakati wote ambao, kutokana makosa yetu wenyewe, hatukumwona. Kristu anatupenda kwa upendo wote usio na mwisho wa moyo wa Mungu mwenyewe.

Tazama jinsi anavyozidi kusisitiza: "Nimekutimizia maombi yako wakati wa msamaha, nimekuletea msaada katika siku ya wokovu."[16] Kwa kuwa anakuahidi utukufu, upendo wake, na anakupa kwa wakati unaofaa; kwa kuwa anatuita, kitu gani utakachompa Bwana, utaitikaje na nitaitikaje, kwa pendo hili la Yesu ambaye amekuja kutulaki?

Siku ya wokovu imewadia. Wito wa mchungaji mwema umetufikia: "Nimekuita kwa jina lako." Maadam pendo halilipwi ila kwa pendo jingine, lazima tujibu: "Mimi hapa, kwa maana umeniita."[17] Nimeamua sitaiacha Kwaresima hii iende kama mvua kwenye jiwe, bila kuacha hata alama. Nitaipa nafasi iniloweshe, inibadili. Nitaongoka, nitamgeukia tena Bwana na kumpenda kama anavyotaka kupendwa.

"Utampenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na roho yako yote na akili yako yote."[18] Na Mtakatifu Agostino asema: "Umebakiwa na sehemu gani ya moyo wako kwa kujipenda mwenyewe? Ni nini kilichobaki katika nafsi yako, kwa akili yako? Anasema ‘wote'. Yeye aliyekuumba anakuhitaji ujitolee kabisa."[19]

60 Baada ya kudhihirisha mapendo yetu hivi, hatuna budi kuishi kama wapenzi wa Mungu. "Katika kila tufanyacho, na tuwe kama watumishi wa Bwana."[20] Ukijitolea kama atakavyo, maongozi ya neema yatadhihirika katika mwenendo wako wa kitaalamu, katika kazi yako, katika juhudi zako za kuvitakatifuza vitu vya kibinadamu — iwe ni vikubwa au vidogo. Kwa maana upendo hukipa kila kitu sura mpya.

Katika kipindi hiki cha Kwaresima, tusisahau kwamba kuwa watumishi wa Mungu si jambo rahisi. Maandishi kutoka kwa waraka wa Jumapili hii yanaendelea: "Kama wahudumu wa Mungu hatuna budi kuwa na subira nyingi, nyakati za mateso, shida; matatizo; tukiwa tunachapwa, gerezani, katikati ya msukosuko; tukiwa tumechoka, kukosewa usingizi na mafungoni. Tunapaswa kuwa na nia safi, wenye nuru, wenye kusamehe na wenye fadhili kwa wengine; hatuna budi kumtegemea Roho Mtakatifu, kwa upendo usioathiriwa, kwa ukweli wa ujumbe wetu, kwa uwezo wa Mungu."[21]

Katika shughuli mbalimbali za siku yetu, katika kila hali, lazima matendo yetu yawe ya watumishi wa Mungu, tukitambua kwamba yu pamoja nasi, kwamba sisi ni watoto wake. Lazima tufahamu mizizi ya Mungu inayojipenyeza katika maisha yetu na kutenda ipasavyo.

Maneno haya ya Mtume yanapaswa kuwafanya muwe na furaha, kwani ni thibitisho la wito wenu kama Wakristu, mkishiriki na watu wengine - wenzenu - shauku, majonzi na shangwe ya maisha ya kibinadamu. Yote haya ni njia inayokwenda kwa Mungu. Analotaka Mungu ni sisi, daima kujifanya watoto na watumishi wake.

Lakini hali hizi za kawaida za maisha zitakuwa njia ya kujitakatifuza tu ikiwa tutajigueza kweli, ikiwa tutajitolea kweli. Kwani Mtakatifu Paulo anatumia maneno yenye ugumu. Anaahidi kwamba Mkristu atakuwa na maisha magumu, maisha ya hatari na ya wasiwasi daima. Tunaupotosha sana Ukristu tukijaribu kuugeuza uwe kitu kitamu na cha kustarehesha! Walakini si kweli kufikiri kwamba njia hii maisha ya kina, na uzito, ambayo imeambatanishwa kabisa na matatizo yote maisha ya mwanadamu, ni kitu kilichojaa uchungu, dhuluma au hofu.

Mkristo ni mpenda kweli. Hali yake ya kiroho na utu wake unamwezesha kufahamu sura zote za maisha yake: dhiki na faraja, mahangaiko yake mwenyewe na ya watu wengine, uhakika na shaka, ukarimu na ubinafsi. Mkristo anapitia haya yote, na anakabiliana nayo yote, kwa uadilifu wa kibinadamu na kwa nguvu anazozipata kutoka kwa Mungu.

Kristu anashawishiwa

61 Kwaresima huadhimisha siku arobaini alizokaa Yesu jangwani akijitayarisha kwa miaka yake ya kuhubiri, iliyofikia kilele cha msalaba na katika ushindi wa Pasaka. Siku arobaini za kusali na toba. Hatimaye: kushawishiwa kwa Kristu, ambako liturjia inatukumbusha katika Injili ya leo.[22]

Kisa chote ni fumbo ambalo mwanadamu hawezi kutumaini kuelewa: Mungu kuhiari kushawishiwa, kumwacha yule mwovu afanye atakavyo. Hata hivyo tunaweza kutafakari, tukimwomba Bwana wetu atusaidie kuelewa fundisho lililomo.

Yesu Kristu kushawishiwa ... Kanisa linataka majaribu ya Kristu yaeleweke hivi: Bwana wetu, aliyekuja kuwa mfano kwetu katika kila jambo, anataka kushawishiwa pia. Na hivyo ndivyo ilivyo, kwa kuwa Kristu alikuwa mwanadamu mkamilifu, kama sisi katika kila kitu isipokuwa dhambi.[23] Baada ya siku arobaini za mfungo, bila chakula kingine licha ya mimea na mizizi na maji kidogo, anahisi njaa - ana njaa sana, kama mtu yeyote angekuwa. Na shetani anapomshauri kwamba ageuze mawe yawe mkate, Bwana wetu sio tu anakataa chakula ambacho mwili wake unahitaji, bali pia anakataa kishawishi kikubwa zaidi: kile cha kutumia uwezo wake wa kimungu kutatua, ikiwa tunaweza kuelezea hivyo, shida ya kibinafsi.

Umegundua jinsi, katika Injili, Yesu hafanyi miujiza kwa manufaa yake mwenyewe. Anageuza maji kuwa divai kwa wageni wa harusi huko Kana;[24] anazidisha mikate na samaki kwa ajili ya umati wenye njaa.[25] Lakini, kwa miaka mingi, anapata mkate wake kwa kazi yake mwenyewe. Na baadaye, wakati wa safari zake kupitia nchi ya Uyahudi, anaishi kwa msaada wa wale wanaomfuata.[26]

Mtakatifu Yohana anaelezea jinsi baada ya safari ndefu wakati Yesu alipofika kwenye kisima cha Sikari, aliwatuma wanafunzi wake mjini kununua chakula. Na anapomwona mwanamke Msamaria anakuja, anamwomba maji, kwa kuwa hana njia ya kuyapata.[27] Mwili wake, ukiwa umechoshwa na safari ndefu, unajisikia mchovu. Mara nyingine anapaswa kulala ili kurejesha nguvu zake.[28] Bwana wetu ni mkarimu kiasi gani katika kujinyenyekeza na kukubali kikamilifu hali yake ya kibinadamu! Hatumii nguvu zake za kimungu kuepuka matatizo au juhudi. Hebu tuombe kwamba atatufundisha kuwa washupavu, kupenda kazi, kutambua utukufu wa kiutu na kimungu inayotokana na kujitolea kikamilifu.

Katika kishawishi cha pili, shetani anapomshauri Yesu ajitose kutoka kwenye mnara wa hekalu, kwa mara ingine, Kristu anakataa ushauri kwamba atumie nguvu zake za kimungu. Kristo hatafuti kilemba cha ukoko, kwa maonyesho. Anatufundisha kutomtumia Mungu kama msingi wa kudhihirisha ubora wetu wenyewe. Yesu Kristu anataka kutimiza mapenzi ya Baba yake bila kutarajia mipango ya Mungu, bila kutenda miujiza kabla ya wakati wake; yumo anakanyaga tu njia ngumu ya binadamu, njia ipendezayo ya msalaba.

Kitu kama hicho kinatokea katika kishawishi cha tatu: anapewa falme, nguvu na utukufu. Shetani anajaribu kuambatanisha tamaa za kibinadamu ibada ambayo inapaswa kuhifadhiwa kabisa kwa Mungu; anatuahidi maisha rahisi ikiwa tutamwangukia mbele yake, mbele ya miungu ya uongo. Bwana wetu anasisitiza kwamba Mungu peke yake ndiye anayestahili kuabudiwa; na anathibitisha nia yake ya kutumikia: "Nenda zako, Shetani; imeandikwa, utamwabudu Bwana Mungu wako, na kumtumikia yeye peke yake."[29]

62 Tunapaswa kujifunza kutokana na msimamo wa Yesu katika majaribu haya. Wakati wa maisha yake hapa duniani hakutaka hata utukufu uliokuwa wake. Licha ya kuwa alikuwa na haki ya kutendewa kama Mungu, alichukua umbo la mtumishi, mtumwa.[30] Na kwa hivyo Mkristo anajua kwamba utukufu wote ni kwa Mungu na kwamba asitumie utukufu na ukuu wa Injili kwa manufaa ya shughuli zake mwenyewe au tamaa za kibinadamu.

Tujifunze kwa Yesu. Msimamo wake dhidi ya utukufu wote wa kibinadamu uko katika uwiano kamili na ukuu wa utume wake wa kipekee kama Mwana mpendwa wa Mungu anayetwaa mwili ili kuwaokoa watu. Ana ujumbe ambao Baba huongoza kwa uangalifu mkubwa: "Wewe ni mwanangu; nimekupata siku ya leo. Omba tu, nawe utapewa mataifa kwa urithi wako."[31]

Na mkristu aliye na msimamo huu, anapomfuasa Kristu, msimamo wa ibada timilifu kwa Baba, vile vile anapata kujua maangalizi ya Bwana yenye upendo: "Ananiamini, yangu ni kumwokoa; anakiri jina langu, kutoka kwangu atakuwa na ulinzi."[32]

63 Yesu anasema "la" kwa shetani, mfalme wa giza. Na mara moja kila kitu ni mwanga. "Kisha shetani akamwacha peke yake; na hapo hapo malaika wakaja na kumtumikia.[33] Yesu kashinda jaribu. Na lilikuwa jaribu halisi, kwa sababu, kwa maoni ya Mtakatifu Ambrosi: "Hakutenda kama Mungu, akitumia nguvu zake. Kama angefanya hivyo, mfano wake ungekuwa na manufaa gani? La. Kama mtu alivyo, anatumia misaada hiyo ambayo nasi ametupa."[34]

Shetani, na nia zake mbaya, alinukuu Agano la Kale: Mungu atatuma malaika wake kumlinda mtu mwenye haki popote aendapo.[35] Lakini Yesu anakataa kumshawishi Babake; anarejesha maana ya kweli kwa aya hii kutoka kwa Biblia. Na, kama thawabu kwa uaminifu wake, wakati unapowadia, watumishi wa Mungu Baba wanajitokeza na kumhudumia.

Inafaa kufikiria juu ya mbinu anayotumia Shetani katika kumshawishi Bwana wetu Yesu Kristu: anaunga hoja zake na kauli kutoka maandiko kutoka kwa vitabu vitakatifu, akipindua na kupotosha maana yao kwa njia ya kufuru. Yesu haachi adanganywe: Neno lililotwaa mwili anajua barabara neno la Mungu, lililoandikwa kwa ajili ya uokovu wa wanadamu - sio kuchanganyikiwa kwao na maangamizi yao. Kwa hiyo, tunaweza kuhitimisha kwamba mtu yeyote ambaye ameungana na Yesu Kristu kwa Upendo kamwe hatadanganywa na upotoshi wa Maandishi Matakatifu, kwa kuwa anajua kwamba ada ya shetani kujaribu kuvuruga dhamira ya Kikristu, kucheza na maneno ya hekima ya milele, akijaribu kugeuza mwanga kuwa giza.

Pindi tuangalie kutokea huku kwa malaika katika maisha ya Yesu, kwa kuwa itatusaidia kuelewa vizuri jukumu lao - utume wao wa kimalaika - katika maisha yote ya mwanadamu. Utamaduni wa Kikristo unaelezea malaika walinzi kama marafiki wenye nguvu, waliowekwa na Mungu kwa kila mmoja wetu, kuandamana nasi katika safari zetu. Ndiyo sababu anatualika kuafikiana nao na kupata msaada kutoka kwao.

Ninaposhauri kwamba tutafakari juu ya vifungu hivi vya maisha ya Kristu, Kanisa linatukumbusha kwamba wakati wa Kwaresima, tunapokiri dhambi zetu, udhaifu wetu na haja tuliyonayo ya kujitakasa, panapo bado nafasi ya shangwe. Kwaresima ni wakati wa ushujaa na furaha; inatupasa kujipa moyo, kwani neema ya Mungu haitatutupa. Mungu atakuwa nasi na atatuma malaika wake kuwa wenzi wetu wa safari, washauri wetu wenye busara njiani, washirika wetu katika yote tunayokabiliana nayo. Malaika "mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe,"[36] kama Zaburi inavyosema.

Inatupasa kujifunza kuzugumza na malaika. Wageukie sasa, mwambie malaika wako mlinzi kwamba maji haya ya kiroho ya Kwaresima hayatatoka rohoni mwako bali yataingia ndani sana, kwa maana unajuta. Waombe wachukue kwa Bwana mapenzi yenu mema, ambayo, kwa neema ya Mungu, yamechipua kutokana na unyonge wako kama yungiyungi aliyepandwa kwenye jaa. Malaika watakatifu, walinzi wetu: "Utulinde katika mapambano ili tusiangamie katika hukumu ya mwisho."[37]

Watoto wa Mungu

64 Unaelezeaje sala hii tumainifu - utambuzi huu kwamba kamwe hatutaangamia katika mapambano? Ni imani inayojikita katika jambo ambalo huwa linanishangaza kila mara: utoto wetu wa kimungu. Bwana wetu, ambaye wakati wa Kwaresima hii anatuomba tubadilike, sio bwana dhalimu au hakimu mgumu asiye samehe: yeye ni Baba yetu. Anazungumza nasi kuhusu utovu wetu wa ukarimu, dhambi zetu, makosa yetu; lakini anafanya hivyo ili kutuopoa navyo, kutuahidi urafiki wake na upendo wake. Utambuzi kwamba Mungu ni Baba yetu huleta furaha kwa uongofu wetu: unatuambia kwamba tunarudi nyumbani kwa Baba yetu.

Utoto huu wa kimungu ni msingi wa madhumuni ya Opus Dei. Watu wote ni wana wa Mungu. Lakini mtoto anaweza kumtegemea baba yake kwa njia nyingi. Lazima tujaribu kuwa watoto wanaotambua kwamba Bwana, kwa kutupenda kama watoto wake, ametuingiza nyumbani kwake, katikati ya ulimwengu, kuwa mojawapo wa jamii yake, ili kile kilicho chake ni chetu, na kile kilicho chetu ni chake, na kukuza ujuzi huo na utumainifu unaotufanya kumwomba mwezi mithili ya watoto!

Mtoto wa Mungu humtendea Bwana kama Baba yake. Yeye si msumbufu na mtumwa, si rasmi tu na mwenye adabu nzuri: anakuwa na moyo mweupe kabisa na mwamini. Watu hawamwaibishi Mungu. Anaweza kuvumilia ukafiri wetu wote. Baba yetu wa mbinguni anasamehe kosa lolote pindi mtoto wake anapomrudia, anapojuta na kuomba msamaha. Bwana ni Baba mwema kiasi kwamba anatazamia shauku yetu kusamehewa na kutusongelea, akifungua mikono yake iliyojaa neema.

Na sasa mimi sijabuni chochote. Kumbuka mfano ambao Yesu alituambia kutusaidia kuelewa upendo wa Baba yetu aliye mbinguni: methali ya mwana mpotevu.[38] "Lakini alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma; akaenda mbio, akamkumbatia shingoni mwake na kumbusu."[39] Hivyo ndivyo maandishi matakatifu yanavyosema: alimfunika kwa busu. Unaweza kutoa maelezo ya kiutu kushinda hayo? Unaweza kuelezea kwa uwazi zaidi mapendo ya mzazi aliyo nayo Mungu kwa watu?

Mungu anapotukimbilia, hatuwezi kukaa kimya, bali tunasema pamoja na Mtakatifu Paulo: Abba, Pater: "Baba, Babangu!"[40] - kwa kuwa, ingawa yeye ndiye muumbaji wa ulimwengu, hajali sisi hatutumii majina ya juu, wala wasiwasi juu ya kutokubali ukuu wake. Anataka tumwite Baba; anataka tupate utamu wa neno hilo, nafsi zetu zikijawa na furaha.

Upande mmoja, maisha ya mwanadamu, ni marejeo ya daima nyumbani kwa Baba yetu. Tunarejea kwa njia ya kitubio, kwa njia ya kuongoka kwa moyo kunako maanisha shauku ya kugeuka, uamuzi wa dhati kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi, ambao kwa sababu hii unadhihirishwa kwa kafara na kujitolea binafsi. Tunarejea nyumbani kwa Baba yetu kwa njia ya sakramenti ile ya msamaha ambayo, kwa kukiri dhambi zetu, tunajivika Yesu Kristu tena na kuwa ndugu zake, watu wa familia ya Mungu.

Mungu anatusubiri, kama baba katika methali, kwa mikono wazi, ingawa hatustahili. Haidhuru deni letu ni kubwa namna gani. Kama vile mwana mpotevu, tunachopaswa kufanya ni kufungua moyo wetu, kutamani kurudi nyumbani kwa Baba yetu, kushangilia na kufurahia katika tunu anayotujalia Mungu kutuwezesha kujiita watoto wake, kuwa watoto wake kweli, hata kama kuitikia kwetu kumekuwa kwa shingo upande.

65 Uwezo gani huu wa ajabu alio nao mwanadamu kusahau hata mambo ya ajabu ya ajabu kupindukia, kuyazoea mafumbo! Tujikumbushe, Kwaresima hii, kwamba Mkristo hawezi kuwa wa juujuu. Wakati akijihusisha kikamilifu katika kazi yake ya kila siku, miongoni mwa watu wengine, walio sawa naye; akiwa mwingi wa shughuli, anaelemewa, Mkristu lazima wakati huo huo anajihusisha kabisa na Mungu, kwa kuwa yeye ni mwana wa Mungu.

Utoto wa kimungu ni ukweli wa kupendeza, fumbo linalofariji. Unajaza maisha yetu yote ya kiroho, unatuonyesha namna ya kuzungumza na Mungu, kumjua na kumpenda Baba yetu aliye mbinguni. Na inafanya mapambano yetu ya ndani kufurika na matumaini na kutupa utumainifu mwelekevu wa watoto wadogo. Zaidi ya hayo: hasa kwa sababu sisi ni watoto wa Mungu, tunaweza kutafakari kwa upendo na mshangao kila kitu kama kuja kutoka kwa mikono ya Baba yetu, Mungu Muumba. Na kwa hivyo tunakuwa watafakari walimwengu, tukiupenda ulimwengu.

Katika Kwaresima, liturjia inakumbuka athari ya dhambi ya Adamu katika maisha ya mwanadamu. Adamu hakutaka kuwa mwana mwema wa Mungu; aliasi. Lakini pia tunasikia sauti ya wimbo wa felix culpa: "’Ee kosa lenye heri,"[41]ambalo Kanisa lote litaimba kwa furaha katika mkesha wa Pasaka.

Mungu Baba, wakati ulipowadia, alimtuma kwa ulimwengu Mwana wake wa pekee, ili kurejesha tena amani; hivi kwamba kwa kuwakomboa watu kutoka kwa dhambi, "tunaweza kuwa wana wa Mungu,"[42] huru kutokana na nira ya dhambi, wenye uwezo wa kushiriki katika undani wa Utatu Mtakatifu. Na hivyo imewezekana kwa mtu huyu mpya, chipukizi hili lililo pandikizwa miongoni mwa watoto wa Mungu,[43] ili kukomboa viumbe vyote kutoka kwa machafuko, kuvirejesha vitu vyote katika Kristu,[44] aliyevipatanisha na Mungu.[45]

Huu basi ni wakati wa toba, lakini, kama tulivyoona, sio jambo hasi. Kwaresima sharti tuishi na moyo wa kujitotosha, ambao Kristo ametugawia na ulio hai katika nafsi zetu.[46] Bwana wetu anatuita tumkaribie zaidi, kuwa kama yeye: "Kuwa waigaji wa Mungu, kama watoto wake wapendwa,"[47] mkishiriki kwa unyenyekevu ila na moyo wenye shauku katika kurekebisha kilichovunjika, kwa kuokoa kilichopotea, kurudisha utaratibu ambapo mwanadamu mdhambi ameharibu, kuongoza kwa lengo lake kile kilichopotoka, ya kurudisha hali sawa ya kimungu miongoni mwa viumbe vyote.

66 Wakati mwingine liturjia ya Kwaresima, na mkazo wake juu ya matokeo ya kumtelekeza Mungu kwa mwanadamu, ina maoni ya msiba, lakini huo sio mwisho wake. Mungu ndiye mwenye neno la mwisho - na ni neno la upendo wa kuokoa na wa rehema, kwa jinsi hii ni neno la utoto wetu wa kimungu. Kwa hiyo, ninawarudieni leo, na Mtakatifu Yohana: "Tazama jinsi Baba alivyotupenda sana; kwamba tuhesabiwe kama watoto wa Mungu, kwa kweli tuwe watoto wake."[48] Wana wa Mungu, ndugu wa Neno lililotwa mwili, wa aliyesemwa, "Ndani yake kulikuwa na uhai, na uhai huo ulikuwa nuru ya mwanadamu."[49] Watoto wa nuru, ndugu wa nuru: ndivyo tulivyo. Tunabeba mwali pekee unaoweza kuwasha moto nyoyo zilizofanywa mwili.

Sasa nitakoma na kuendelea na Misa, na nataka kila mmoja wetu afikirie kile Mungu anachotaka kwake, makusudio gani, ni maamuzi gani neema inataka iyahimize ndani mwake. Na mnapo angalia matakwa haya ya kujitolea na mapambano yanayoendelea, kumbukeni kwamba Yesu Kristu ni mfano wetu. Na kwamba Yesu, akiwa Mungu, aliacha ashawishiwe, kusudi tuweze kuwa na moyo bora zaidi na kuwa na uhakika wa kushinda. Kwa Maana Mungu hashindwi pambano lolote, na ikiwa tumeungana naye, hatutashindwa kamwe. Kinyume chake, tunaweza kujiita washindi na kwa kweli kuwa washindi: watoto wema wa Mungu.

Tuwe na furaha. Nimefurahi. Sipaswi kufurahi, nikiyaangalia maisha yangu, nikifanya ule uchunguzi wa dhamira yangu binafsi unaotakiwa na Kwaresima. Na hata hivyo nafurahi, kwani ninatambua kwamba Bwana ananitafuta tena, kwamba Bwana bado ni Baba yangu. Najua kwamba wewe na mimi hakika tutatambua, kwa nuru na msaada wa neema, vitu gani lazima vichomwe na tutavichoma; vitu gani lazima ving’olewe na tutaving’oa; vitu gani viachwe na tutaviacha.

Si rahisi. Lakini tuna mwongozo dhahiri, ambao isingefaa tuwe bila na hatuwezi kuwa bila nao. Tunapendwa na Mungu, nasi tutamwacha Roho Mtakatifu atende kazi ndani yetu na kututakasa, ili tuweze kumkumbatia Mwana wa Mungu msalabani, na kufufuka naye, kwa vile shangwe ya ufufuko imekita mizizi msalabani.

Maria, Mama yetu, "msaada wa Wakristo, kimbilio la wakosefu": mwombe Mwanao atutumie Roho Mtakatifu, aamshe katika mioyo yetu uamuzi wa kuendelea kwa ujasiri, akitufanya tusikie ndani rohoni mwetu wito ulioujazia amani ushahidi wa dini wa mmoja wa Wakristu wa awali: wito ambao ulijaza amani ya kifo cha shahidi wa mmoja wa Wakristo wa kwanza: "Njoo, urudi kwa Baba yako,"[50] anakusubiri.

[1] Mafundisho yaliyotolewa 2 Machi, 1952, Jumapili ya kwanza ya Kwaresima.

[2] Zaburi 90:15 Invocabit me et ego exaudiam eum

[3] Zaburi 50:19

[4] Zaburi 90:15

[5] Zaburi 90:1: Eripiam habitat in adiutorio Altissimi, in protectione Dei coeli commorabitur

[6] Yohana 3:30: Illum oportet crescere, me autem minui

[7] Wagalatia 2:20

[8] Sermo 169,15 (PL 38,926)

[9] Luka 9:23

[10] Epistola 121,3 (PL 22,1013)

[11] Waefeso 5:8-10

[12] 2 Wakorintho 6:1 (waraka wa Misa) Exhortamur ne in vacuum gratiam Dei recipiatis

[13] Wagalatia 6:7

[14] 2 Wakorintho 6:2 (waraka wa Misa)

[15] Isaya 43:1: Ego vocavi te nomine tuo

[16] 2 Wakorintho 6:2 (waraka wa Misa)

[17] 1 Sam 3:5 Ecce ego quia vocasti me

[18] Mathayo 22:37

[19] Sermo 34,4,7 (PL 38,212)

[20] 2 Wakorintho 6:4 (waraka wa Misa): In omnibus exhibeamus nosmetipsos sicut Dei ministros

[21] 2 Wakorintho 6:4-7

[22] cf Mathayo 4:1-11

[23] cf Waebrania 4:15

[24] cf Yohana 2:1-11

[25] cf Marko 6:33-46

[26] cf Mathayo 27:55

[27] cf Yohana 4:4 ffcf

[28] cf Luka 8:23

[29] Mathayo 4:10

[30] cf Wafilipi 2:6-7

[31] Zaburi 2:7: Filius meus es tu, ego hodie genui te. Postula a me et dabo tibi gentes hereditatem tuam

[32] Zaburi 90:14 (njia ya Misa)

[33] Mathayo 4:11

[34] Expositio Evangelii secundum Lucam, 1,4,20 (PL 15,1525)

[35] Zaburi 90:11 (njia ya Misa)

[36] Zaburi 90:12 (njia ya Misa): In manibus portabunt te, ne forte offendas ad lapidem pedem tuum

[37] Missale Romanum, sala ya Mtakatifu Mikaeli: Defende nos in proelio, ut non pereamus in tremendo iudicio

[38] cf Luka 15:11 ff

[39] Luka 20

[40] Warumi 8:15

[41] Missale Romanum, paschal Praeconium

[42] Wagalatia 4:5: adoptionem filiorum reciperemus

[43] Tazama Warumi 6:4-5

[44] Tazama Waefeso 1:5-10

[45] Tazama Wakolosai 1:20

[46] Tazama Wagalatia 4:6

[47] Waefeso 5:1

[48] 1 Yohana 3:1

[49] Yohana 1:4

[50] Mtakatifu Ignatio wa Antiokia, Epistola ad Romanos, 7,2 (PG 5,694): Veni ad Patrem